
Katibu Mkuu wa Wizara ya afya Dkt. John Jingu amewataka wataalam wa afya kuandaa mpango mkakati madhubuti utakaokua ni muongozo katika kutoa huduma za afya nchini na kuwafikia wananchi popote walipo ikiwemo kuangalia fursa za kiuchumi ndani na nje ya nchi.
Dkt. Jingu amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na taasisi binafsi imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya hivyo anategemea uwekezaji huo ulete matokeo Chanya kwa nchi hivyo wataalam wanatakiwa kuchangamkia masoko ya ndani na nje.
Dkt. Jingu amesema hayo wakati akifungua kikao cha Wataalam mbalimbali wa afya waliokutana jijini Dodoma kwa ajili ya kuandaa mpango wa Wizara ya Afya wa kuboresha utoaji wa huduma za nchini.
Dkt.Jingu ameongeza kuwa sekta ya afya kazi yake sio kutoa huduma peke yake kwa wagonjwa au kuzuia na kupambana na magonjwa bali inatakiwa iwe chanzo cha ukuaji wa uchumi wa nchi hivyo amewataka wataalam hao kuweka mikakati itayofungua fursa za kiuchumi kupitia afua mbalimbali za afya.
Dkt. Jingu amesema kuna fursa nyingi katika ukanda wa Afrika Mashariki, kusini mwa jangwa la sahara, Afrika na duniani kwa ujumla kuhusu masuala ya afya akitolea mfano mkataba wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) na Bohari ya Dawa (MSD) kuhusu kununua, kuuza na kusambaza bidhaa za dawa kwenye nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuwa ni mojawapo ya fursa ya kiuchumi Tanzania inayonufaika nayo.
Amesema kupitia mikataba mbalimbali nchi iliyojiwekea inaweza kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa nchi hivyo amewataka wataalam hao kujadili na kuandaa mkakati wa Wizara utakaokua ni chachu ya kusukuma ukuaji wa uchumi kwa kuchungulia fursa zilizopo.
