Back to top

WATOTO 24 WAFANYIWA UPASUAJI WA MOYO JKCI

12 September 2023
Share

Watoto 24 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo, wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo, katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo inayoendelea, katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Kambi hiyo ya upasuaji inafanywa na wataalamu wa upasuaji wa moyo, kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu cha nchini Saudi Arabia.

Akizungumza kuhusu kambi hiyo, Mkuu wa kitengo cha upasuaji wa moyo kwa watoto wa JKCI Dkt. Godwin Sharau, alisema licha ya kufanya kambi hiyo ya matibabu wamepata pia fursa ya kujifunza mbinu mpya za kitabibu na kuongeza ufanisi, wa namna ya kufanya kazi kwa haraka katika muda mfupi hivyo kuweza kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi.

Dkt. Sharau ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto alisema baadhi ya watoto ambao wamefanyiwa upasuaji ni wale waliozaliwa na matundu katika moyo, watoto ambao valvu zao hazijajitengeneza vizuri na wengine ambao mishipa yao ya damu haijakaa katika mpangilio wake.