
Waziri wa Afya, Mhe.Ummy Mwalimu, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt.Francis Michael, kuwahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kuwalipa watumishi wa Afya stahiki zao kwa wakati.
.
Mhe.Ummy ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na wajumbe wa Timu za Usimamizi na Uendeshaji wa Huduma za Afya ngazi ya Mkoa (RHMT), alipokuwa akihitimisha ziara yake katika Mkoa huo, Septemba 13, 2023.
.
“Naomba sana Mhe. Mkuu wa Mkoa kupitia kwako kuwahimiza Wakurugenzi kuwalipa watumishi wa Afya stahiki zao kwa wakati ili wapate moyo wakuendelea kutoa huduma katika vituo vyetu vya Afya”. Amesema Waziri Ummy.
.
Waziri Ummy amesema Wakurugenzi wengine waige mfano kwa Mkurugenzi wa Momba ambaye amewagawia viwanja watumishi wa Afya hivyo, lazima kuwajengea motisha na kuwavutia watumishi hao wa Afya ili waendelee kufanya kazi katika Halmashauri za Mikoa.
.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt.Francis Michael amemuomba Waziri huyo, kupeleka watumishi wa Afya hasa madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.
.
“Hili ni jambo kubwa sana Mhe. Waziri tunakuomba sana utuletee madaktari bingwa katika Mkoa wetu, haya mengine ya fedha Mhe. Rais ametuletea fedha nyingi na bado anaendelea kuleta ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi”. Amesema Dkt. Michael
