
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, amesema kampeni ya upandaji wa Malisho ya mifugo, uchimbaji wa visima na malambo katika mashamba binafsi ya wafugaji unakwenda kutatua tatizo la migogoro ya ardhi iliyopo kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hasa wakulima.
Amewataka wafugaji kumiliki maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kufuata sheria na taratibu zilizopo ili wasiingie kwenye migogoro ambayo inaweza kusababisha uvuvnjifu wa amani.
Naibu Waziri Mnyeti amesema kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikijitokeza kutokana na kutokuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Vijiji na kwenye maeneo ambayo tayari mipango hiyo usimamizi wake unakuwa hafifu, Hivyo amewasihi viongozi wa Mvomero kuhakikisha Vijiji vinakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuusimamia.
Mnyeti amewaeleza wafugaji kuwa Wizara kwa sasa imejipanga kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mwananchi hivyo ikiwa kosa linakuwa kwa mfugaji au mkulima basi kila mmoja atachukuliwa hatua kulingana na sheria na taratibu zilizopo.
