Back to top

DCEA: YAENDESHA OPERESHENI BONDE LA MTO MARA

09 October 2023
Share

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni maalum mkoani Mara hususani katika kanda maalum ya Tarime Rorya kwenye bonde la mto Mara.
 
Akizungumzia wakati wa operesheni hiyo , Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, wakazi wa eneo hilo wamelifanya bonde la mto Mara kama eneo maalum kwa ajili ya kilimo cha bangi na kujimilikisha kwa kutoruhusu mtu yeyote asiye mkazi kuingia kwenye bonde kama sehemu ya kuficha uharifu wao.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema jumla ya gunia 507 za bangi kavu iliyo tayari kusafirishwa, gunia 50 za mbegu za bangi pamoja na  kuteketeza viwanda viwili vidogo vilivyokuwa vikitumika kuchakata na kufunga bangi kabla ya kusafirishwa ambapo watuhumiwa 11 wanashikiliwa kuhusika na dawa hizo.

Kwa upande wake Diwani Kata Ya Tulwa Chacha Machugu amesema, Viongozi wa Serikali za Mitaa wanaosaidia kuendelea kwa kilimo cha bangi wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine. Aidha, amewaomba viongozi wa dini kusaidia kuwaambia waumini wao kuwa dawa za kulevya hazitakiwi.

Huku baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Tarime, wamepongeza juhudi za serikali katika kutokomeza dawa za kulevya nchini na wameiomba serikali kufanya operesheni endelevu na kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya kwani dawa hizo zimekuwa zikiathiri vijana kwa kiasi kikubwa.