
Serikali imesema imejidhatiti katika kuhakikisha inalipa madeni ya makandarasi wa ndani ,baada ya maelekezo ya Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kuagiza madeni hayo yalipwe kwa haraka.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Mwanza na Waziri wa Ujenzi Mhe.Innocent Bashungwa, wakati wa mkutano na Makandarasi katika mafunzo ya kozi maalumu ya usimamizi wa mkataba yaliyoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kwa makandarasi wa mikoa ya kanda ya ziwa ambayo ni Mwanza, Geita, Kagera, Simiyu, Shinyanga na Mara.
Bashungwa amesema,"Serikali haipendezwi na hali hiyo na inajitahidi kuitatua kwa mfano, Mheshimiwa Rais, ameagiza madeni yote ya nyuma ya makandarasi yalipwe. Kuanzia mwezi Agosti 2023, Serikali hutenga TZS 70 bilioni kwa lengo la kulipa madeni ya makandarasi. Katika hizo, TZS 50 bilioni zinalipwa kwa makandarasi wa ndani na TZS 20 bilioni kwa makandarasi wageni.



Waziri Bashungwa amesema ni kupitia mpango huo hadi kufikia mwezi Novemba 2023, madeni yote ya makandarasi yatakuwa yameshalipwa.
Kauli hiyo ya waziri Bashungwa ameitoa kufutaia maombi ya mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Mhandisi Joseph Nyamhanga ya kuomba serikali kwa niaba ya makandarasi kutatua changangoto ya ucheleweshwaji wa malipo kwa makandarasi, hali ambayo imekuwa ikikwamisha utendaji wa makandarasi katika ukamilishaji wa miradi kwa wakati.
Nyamhanga amesema , "Mheshimiwa Waziri changamoto hii ni kubwa na inawaathiri sana makandarasi wa ndani na hivyo ninaomba uichukue na kuona jinsi ya kuitatua".

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Makandarasi mhandisi Rhoben Nkori amesema Bodi hiyo inafanyia kazi maelekezo ya wizara na kutengeneza mpango mkakati wa kuwawezesha makandarasi wa ndani kupata zabuni zinazotolewa na serikali.
Mkutano huo pia umelenga kutoa mafunzo kwa makandarasi ya mfumo mpya wa manunuzi kwa njia ya mtandao (NeST).
