Back to top

WATU SITA WAFARIKI KATIKA AJALI MAKETE, MKOANI NJOMBE.

14 October 2023
Share

Watu sita wamefariki dunia na wengine kumi na mmoja kujeruhiwa katika ajali ya gari ya abiria Toyota haisi lenye namba za usajili T733 BBP  baada ya kupinduka katika kijiji cha Ndulamo wilaya ya Makete, Mkoani njombe baada ya dereva wa gari hilo kushindwa kukata kona na kupinduka usiku wa kuamkia leo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe, Kamishina Msaidizi wa Polisi John Imori, amesema gari hiyo ilikuwa imebeba abiria kumi na nane na chanzo cha ajali ni mwendo kasi.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt.Juma Mfanga amethibitisha kupokelewa kwa majeruhi na kutokea kwa vifo hivyo.

Ajali hiyo pia imewagusa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoani Njombe, ambao baadhi walitumia gari hiyo kusafiri kurudi katika makazi yao baada ya kumaliza ziara ya siku Moja ya mlezi wa CCM mkoa wa Njombe, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu CCM Taifa katika Wilaya ya Makete Bi.Halima Mamuya.