Back to top

KISWAHILI CHAPIGIWA CHAPUO MIKUTANO YA WB NA IMF

15 October 2023
Share

Tanzania imeishauri Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kukifanya kiswahili kuwa miongoni wa lugha za mawasiliano wakati wa mikutano yake kutokana na kukua kwa lugha hiyo na kutumika kwenye mikutano mingine mingi ya Kikanda na Kimataifa.

Ushauri huo umetolewa Mjini Marrakesh nchini Morocco, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, wakati wa Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia.


“Takribani watu milioni 200 wanazungumza Kiswahili duniani, tumewasilisha ombi hili ikiwa ni jitihada za Serikali za kukibidhaisha Kiswahili saw ana lugha nyingine zinazotumika kama lugha rasmi kwenye mikutano ya Benki ya Dunia na IMF), alisema Dkt. Saada Mkuya Salum

Agenda hiyo itajadiliwa wakati wa Mkutano wa 27 wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia, wakati wa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), itakayofanyika Washington D.C, nchini Marekani, Mwezi Aprili, Mwakani.