
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka wataalam sekta za mifugo na uvuvi kuongeza ubunifu katika shughuli zao za kila siku ili mchango wa sekta hizo katika uchumi wa Taifa uweze kuongezeka tofauti na ilivyo sasa ambapo sekta ya uvuvi inachangia asilimia 1. 8 na sekta ya mifugo inachangia asilimia 7.0.
Waziri Ulega ameyasema hayo leo, wakati akifungua kongamano la 46 la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo linaloenda sambamba na mkutano mkuu wa 47 wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP), linalofanyika jijini Arusha.



Aidha, Ulega amewataka wataalam hao kutambua kuwa wanajukumu kubwa la kuendeleza sekta hizo, na kwamba huu ni wakati mwafaka wa kufanya mapinduzi makubwa katika minyororo ya thamani ya mifugo na samaki ili kukidhi mahitaji ya chakula na lishe bora ndani na nje ya nchi.
"Wizara ninayoisimamia inatia mkazo kwenu wataalamu muweke nguvu katika taaluma zenu ili kuongeza uzalishaji wa mifugo na samaki kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi"Amesema Ulega
Amendelea kufafanua kuwa Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa, ilikuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula ya Afrika (AGRF) mwaka huu, ambapo wadau wote duniani walikubaliana kusimamia mabadiliko ya mifumo ya chakula na kuongeza uzalishaji na kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa wote.
Hivyo, aliitaka TSAP na wanachama wote kuendelea kuunga mkono makubaliano hayo ambayo Serikali imeazimia kuyatekeleza kwa vitendo.
Naye Mwenyekiti wa TSAP, Dk Jonas Kizima amesema moja ya malengo ya chama hicho ni kuhimiza maendeleo katika sayansi ya uzalishaji wa mifugo na uvuvi hapa nchini.
