
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson Mwansasu, amechaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), katika uchaguzi uliofanyika leo Jijini Luanda nchini Angola katika mkutano wa 147.
Dokta Tulia ameshinda urais huo baada ya kupata kura 172 kati ya kura 303 zilizopigwa katika uchaguzi huo hivyo ana chukua nafasi ya rais aliyemaliza muda wake, Duarte Pacheco kutoka nchini Ureno.
Wagombea wengine walioshiriki katika uchaguzi huo ni Catherine Hara, kutoka Malawi aliyepata kura 61, Adji Diarra kutoka Senegal aliyepata kura 51 na Marwa Hagi kutoka Somalia aliyepata kura 11.
Katika maelezo yake wakati akiomba kura, Dkt.Tulia amewaahidi wapiga kura na nchi wanachama wa bunge hilo , kuwa atasimamia misingi ya umoja kwa kuongeza ufanisi, uwajibikaji na uwazi katika bunge hilo la Dunia.
Akizungumza na Vyombo vya Habari baada ya kushinda nafasi hiyo, Spika wa Bunge, Dkt.Tulia amesema ushindi huo ni heshima kubwa kwa Tanzania na inaonesha jinsi inavyoheshika na kutambuliwa duniani katika masuala mbalimbali ikiwemo nafasi yake katika bunge hilo la dunia.
