
Jeshi la polisi mkoani Kagera limefanikiwa kumtia mbaroni Deogratias Simon ambaye ni mwalimu shule ya sekondari Nyakisasa iliyoko wilayani Ngara mkoani Kagera aliyekuwa anatafutwa na jeshi hilo tangu mwaka 2016 kwa tuhuma ya kusambaza ujumbe kwenye mitandao ya kijamii uliokuwa unalenga kumkashifu Dkt.John Pombe Magufuli ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ofisini kwake,Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera, Kamishina Msaidizi Mwandamizi,Augustine Ullomi amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa na Jeshi hilo jana kufuatia uchunguzi uliofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama katika mkoa huo, kamanda huyo ameeleza kuwa mtuhumiwa aliyekamatwa alikuwa amkashifu Rais Magufuli kupitia ukurasa wake wa facebook kwa kusambaza ujumbe kwamba rais huyo ni dikteita na anaiminya demokrasia.
Aidha,Kamanda Ullomi ametoa onyo kwa wanaowakashfu viongozi wakuu wa serikali kupitia kwenye mitandao ya kijamii,ameahidi kuwa jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama litaendelea kuwasaka popote pale walipo na kuwachukulia hatua kali hivyo akawaomba wananchi wawafichue wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kuwakashfu viongozi wakuu wa serikali kwa kuwa jeshi hilo linataka kukomesha vitendo hivyo.