Back to top

ULEGA AKABIDHI BOTI ZA BIL.1 KWA WAVUVI TANGA

05 November 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekabidhi Boti za kisasa 14 za uvuvi zilizotolewa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya kuwapa wavuvi Mkoani Tanga ili wazitumie kuboresha shughuli zao.
.
Akikabidhi boti hizo, Mhe. Ulega amesema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha maisha ya wavuvi na ndio maana anatoa pesa nyingi kwa ajili ya kuziwezesha sekta za uzalishaji ikiwemo sekta ya uvuvi ziweze kutekeleza majukumu yake kwa weledi na  ufanisi ili kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zikiwemo za uvuvi zinazidi kunufaisha Taifa na Watanzania kwa ujumla.


Ulega ameeleza hayo mkoani Tanga na kusema mpango huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambapo katika awamu ya kwanza jumla ya boti 160 zenye thamani ya shilingi Bilioni 11.5 zitatolewa kwa wanufaika nchi nzima huku zikitarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa takriban watu 4,296 wakiwemo wavuvi mmoja mmoja, vikundi na vyama vya ushirika.  
.
Ulega pia amekemea vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea huku akisisitiza kuwa boti hizo zilizokabidhiwa leo, ni mahsusi kwa ajili ya uvuvi endelevu tu na si vinginevyo, na kwamba, Serikali haitosita kuchukua hatua za kisheria ikigundua wavuvi wanajihusisha na uvuvi haramu au usafirishaji wa mazao haramu ya uvuvi.  
.
Awali Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Agnes Meena alisema boti hizo za kisasa zimetokana na mkopo nafuu usiokuwa na riba kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) ambao wanashirikiana na serikali kuhakikisha wanakuza pato la wavuvi.
.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amemshukuru Rais, Dkt Samia kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuliongoza Taifa  na kuliletea maendeleo ikiwemo boti hizo 14 zilizotolewa kwa mkoa wa Tanga ambazo zitasaidia kusukuma mbele maendeleo ya wavuvi.