
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kufanya majaribio ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika Kata ya Ng'ambo iliyopo Manispaa ya Tabora yenye vituo 10 na Kata ya Ikoma yenye vituo 6, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara kuanzia Novemba 24-30, 2023.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Mhe.Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele, katika Mkutano wa Kitaifa wa Tume ya Uchaguzi na vyama vya siasa kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.
.
Jaji Mwambegele amesema lengo la majaribio hayo ni kupima uwezo na ufanisi wa vifaa, pamoja na mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi Hilo nchi nzima.
.
Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw.Ramadhani Kailima, amesema zoezi hilo litafanyika kwa siku 7 katika maeneo yote kuanzia Saa 2 :00 Asubuhi Hadi saa 12:00 Jioni.

Ameongeza kuwa uboreshaji wa majaribio utahusisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi na atayetimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, wapiga kura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo jingine, waliopoteza au kadi zilizoharibika, wanaorekebisha taarifa zao na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari.
