
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega, amesema katika bajeti ya mwaka 2024/25 mpango wa Serikali kupitia Wizara yake ni kuendelea kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika sekta ya uvuvi ili kuiwezesha kuchangia katika Pato la Taifa kwa Asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
Waziri Ulega amesema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Uvuvi Duniani yanayofanyika leo Zanzibar.
"Malengo yetu ifikapo mwaka 2030 sekta ya uvuvi iwe na uwezo wa kuchangia asilimia 10 kutoka wastani wa asilimia 1.8 ambayo inachangia hivi sasa,"Amesema Ulega.
Amesema anawashukuru sana Mhe.Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan, na Mhe. Rais, Dkt. Hussein Ally Mwinyi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuziwezesha sekta za uvuvi Tanzania Bara na Zanzibar na namna wanavyowapa wavuvi nchini kipaumbele cha hali ya juu.
Ameongeza kwa kusema kuwa katika jitihada za Serikali kuiwezesha sekta ya uvuvi kuendelea kutoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa, Mhe. Rais, Dkt. Samia ametoa boti 160 pamoja na vifaa vyake ili wavuvi waweze kufanya shughuli zao kisasa.
Amesema kwa hatua hiyo ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa boti 160 imewafurahisha wavuvi kwani wanaamini boti hizo zitawasaidia kufanya shughuli zao kwa uhakika na kukuza kipato chao.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Uvuvi Duniani yanayofanyika Zanzibar yalifunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah.
