Back to top

RAIS SAMIA HAKUNIPA KAZI YA KUMEGA ARDHI ZA WATU

25 November 2023
Share


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Jerry Silaa, amesema hakuteuliwa na Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kumega ardhi za watu wanaomiliki kihalali kwa ajili ya kuwagawia wananchi waliovamia maeneo.

Waziri Silaa amesema hayuko tayari kunyang'anya na kumega ardhi za watu wanaomiliki kwa haki na wana hati zao za kumiliki ardhi kwa ajili tu ya kuwapa wavamizi wa maeneo hapa nchini.

Waziri Silaa amesema hayo wakati akipokea taarifa ya kamati ya siku sita ya utatuzi wa mgogoro wa wakazi wa kijiji cha Sikaungu na Mwekezaji wa shamba la Efatha katika kikao cha Kamati ya Usalama ya mkoa wa Rukwa.

Silaa ametilia mkazo kauli hiyo baada ya kupokea maoni mbalimbali ya viongozi walioshiriki kikao hicho ambapo moja ya maoni aliyoyapinga ni ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Sumbawanga
Gerald Kalolo Ntila.

Mwenyekiti huyo wa Halmashauri alimuomba Mhe. Waziri Silaa kumega baadha ya hekari kutoka katika shamba hilo na kuwagawia wananchi ambao wanalizunguka shamba hilo na wanauhitaji wa ardhi.

Ziara ya Waziri Silaa inakuja baada ya mwishoni mwajuma lililopita kufika Kijijini hapo kuwasikiliza wananchi na kisha kuunda Kamati ambayo inatakiwa kuwasilisha ripoti yake hii leo kwa lengo la kumaliza mgogoro huo.

Mgogoro wa wananchi hao wa Sikaungu moja kijiji kinachopakana na shamba la Efatha ulianza mara baada ya shamba hilo ambalo lilikuwa la serikali chini ya DAFCO kabla ya kutangazwa kuuzwa mnamo mwaka 2006 na kununuliwa na Efatha ilihali kukiwa na kutofautiana mitazamo juu ya mipaka ya shamba hilo baina Mwekezaji na wakazi wa kijiji hicho.

 Shamba la Efatha lenye ukubwa wa zaidi ya Hekta Elfu kumi linapakana kwenye halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga na ile halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga ambayo limo kwenye vijiji vya Sikaungu, Songambele na Msandamuungano