Back to top

SERIKALI KUGHARAMIA MAZISHI, MAJERUHI MANYARA. 

04 December 2023
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amemuelekeza Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, kuwa serikali igharamie mazishi ya wote waliopoteza maisha kutokana na mvua kubwa iliyotokea na mafuriko katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang.

Rais Samia pia ametaka majeruhi wote ambao wapo kwenye hospitali mbalimbali wapate matibabu yote yanayostahili kwa gharama za Serikali, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea kutoa msaada wa dharura na uokoaji.

Aidha Rais Samia ameelekeza Serikali ya mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu, kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda kwa ajili ya kuwastiri wananchi hao.

Wakati huo huo Rais Samia ameelekeza tathmini ya kina ifanyike juu ya maafa hayo na vitengo na taasisi zote za Serikali zinazohusika kuwepo eneo la tukio na kufanya  kazi usiku na mchana ili kuhakikisha hali inarejea kawaida.

Rais Samia ametoa pole kwa wafiwa wote kutokana na msiba mkubwa uliowakumba na pia anawahakikishia wananchi walioathirika kuwa serikali iko pamoja nao na itahakikisha inashughulikia masuala yote yaliotokana na janga hili.

Rais Samia ambaye amekuwepo Dubai kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) ameamua kufupisha safari hiyo na kurejea nchini haraka iwezekanavyo, ili kushughulikia kwa karibu janga hilo.