Back to top

WATU WALIOFARIKI KUTOKANA NA MAPOROMOKO MANYARA WAFIKIA 65

05 December 2023
Share

Waziri Mkuu, Mhe.Kassim Majaliwa, ameshuhudia kazi ya kusomba matope kwenye mji mdogo wa Katesh, Wilayani Hanang, Mkoani Manyara, ikianza kwenye barabara kuu ya kutoka Babati hadi Singida.

Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji huo, Waziri Mkuu amesema idadi ya watu waliokufa katika maafa hayo imefikia watu Sitini-na-Watano.

Ametumia fursa hiyo kuwafikishia salamu za pole kutoka kwa Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan na kwamba amekatisha ziara yake nje ya nchi  na yuko njiani kurejea nyumbani na kesho-kutwa atazuru maeneo yaliyoathirika na kutoa pole kwa waathirika.

Mapema, Waziri Mkuu aliwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na kutembelea wodi ya watoto, wanaume na wanawake.

Pia alikutana na timu ya Madaktari Bingwa kutoka Dodoma na Arusha inayoongozwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,  Dkt.Ernest Ibenzi ambaye amesema timu yake ina watu 21 wakiwemo madaktari bingwa  Kumi-na-Wawili ambapo sita wanatoka Dodoma na wengine sita wanatoka Arusha.