
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geofrey Pinda amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga kuunda timu maalum ya kufanya tathmini kwa vyuo vyake vya Ardhi Tabora na Morogoro na kushauri namna bora ya kuboresha vyuo hivyo
Ametoa siku saba kuanzia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi kuunda timu hiyo haraka itakayofanya ukaguzi wa mahesabu, makusanyo ya mapato ya ndani na kutoa ushauri pamoja na mambo mengine namna bora ya kutumia mapato ya ndani kwa ile miradi ya maendeleo.
Aidha, timu hiyo itaangalia pia suala la ajira kwa watumishi ambapo kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi vyuo hivyo vya ardhi vinatumia wastani wa Shilingi milioni 80 hadi 100 kwa walimu wa muda pekee kiasi alichokieleza ni kikubwa.
Pinda ametoa agizo hilo kwenye Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) mkoani Tabora.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARITA) Dkt Lucy Shule, amemueleza Naibu Waziri Pinda kuwa, Chuo hicho cha Ardhi kinakabiliwa na upungufu wa watumishi, vyumba vya madarasa, Maabara pamoja na vyumba vingine vya mafunzo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Ushauri ya ARITA, ubora wa wahitimu na mafanikio ya wanafunzi wa chuo hicho inategemea sana ubora wa program na kozi walizozisoma pamoja na mchakato wa mafunzo kwa vitendo waliyoyapitia.
Ameiomba Wizara ya Ardhi kukiongezea chuo hicho vitendea kazi vya kujifundishia alivyovieleza kuwa vitawasaidia wanafunzi kupata ujuzi na stadi zilizolengwa katika mafunzo yao na kuwawezesha kuwa na umahiri katika kufanya kazi zao kwa kujiamini na ubora unaokidhi viwango vya mahitajio ya soko.
Jumla ya wahitimu 1,132 wametunukiwa Astashahada na Stashahada katika fani za Usimamizi wa Mazingira, Mifumo ya Taarifa za Kijiofrafia, Sanaa, Ubunifu na uchapishaji, Urasimu Ramani pamoja na Usimamizi wa Ardhi, Uthamini, na usajili.
