Back to top

WAZIRI ULEGA:WAKULIMA TENGENI MAENEO YA KULIMA MALISHO.

14 December 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahimiza wafugaji kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya kulima malisho  ili kuwa na uhakika wa malisho kwa ajili ya mifugo yao wakati wote.

Waziri Ulega ametoa wito huo alipotembelea shamba la mbegu na malisho la wizara hiyo lililopo  Vikuge, Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani,  Shamba hilo ni miongoni mwa mashamba ya malisho ya mifugo ambayo Serikali imefanya uwekezaji mkubwa. 

Wakati akikabidhi mbegu za malisho za aina ya Juncao kwa baadhi ya wafugaji waliofika shambani hapo ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wafugaji kuona umuhimu wa kulima malisho, Waziri Ulega amesema kuwa kila mfugaji ni muhimu awe na eneo la malisho kwani itawasaidia kuondokana na migogoro baina yao na wakulima.

Mheshimiwa Ulega amesema katika shamba hilo kuna tani 78 za mbegu za majani aina ya Juncao ambayo ni bora kwa ajili ya kuzalisha malisho ya mifugo.Amewataka wafugaji kupanda mbegu hizo ili kuondokana na changamoto ya kuvamia mashamba ya wakulima.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza, amesema kuwa mbegu hizo za Juncao zilizopo katika shamba la Vikuge litasaidia kupunguza changamoto ya malisho huku akisema kuwa mpango wa Wizara ni kusambaza mbegu za malisho hayo katika mashamba mengine ya Wizara yaliyopo mikoani ili kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi