Back to top

HUDUMA ZA AFYA MIPAKANI KUENDELEA KUIMARISHWA

14 December 2023
Share

Serikali imegawa magari 16 yakiwemo magari matatu  ya kubebea wanaohisiwa kuwa na magonjwa ya kuambukiza, pamoja na Pikipiki 20, ikiwa ni hatua ya kutatua changamoto ya usafiri kwa watumishi na kuongeza kasi ya huduma za Afya, kwenye maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege nchini. 
.
Akizungumza katika Hafla ya kukabidhi magari hayo, iliyofanyika katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Mkoani Kilimanjaro, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, amesema Serikali  imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za kudhibiti magonjwa kuenea ndani ya nchi na kuzuia yasiingie au kuenea nje ya mipaka ya nchi.
.
Mollel, amesema kwa wastani jumla abiria 114,000 kwa mwezi huwasili nchini kutoka nchi mbalimbali na pia wastani wa abiria 86,800 kwa mwezi husafiri nje ya nchi hasa kupitia uwanja wa ndege JNIA, Kiwanja cha ndege Kilimanjaro (KIA) pamoja na mipaka ya Namanga, Tunduma, Rusumo, Kasumulu na Mutukula.

Kwa kuzingatia umuhimu huo Wizara ya Afya inaendesha huduma za afya katika mipaka 54 inayojumuisha Viwanja vya ndege 13, Bandari 12 na Mipaka ya nchi kavu 29, ambapo huduma zinazotolewa ni pamoja na Chanjo ya homa ya manjano, upimaji wa afya za abiria pamoja na ukaguzi wa bidhaa mbalimbali ili kudhibiti kuenea kwa magonjwa.