Back to top

ULEGA: SAMIA NI 'CHAMPION' WA NISHATI SAFI AFRIKA

15 December 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga amesema kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwa kinara wa kuwakomboa kina mama kiuchumi kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuwafanya waondokane na  matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamekuwa na athari kwa mazingira na afya ya binadamu.

Waziri Ulega amesema hayo wakati wa Kongamano la Wanawake Wilaya ya Mkuranga lililofanyika Wilayani hapo katika Mkoa wa Pwani.

Amesema kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia alipokuwa kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP 28) uliofanyika Dubai mapema Mwezi Novemba, 2023, alitumia fursa hiyo kuielezea Dunia kuhusu dhamira yake ya dhati ya kuwawezesha Wanawake kujikwamua kiuchumi kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameongeza kuwa mitungi hiyo ambayo thamani yake ni Shilingi Milioni 57 itagawiwa kwa  Walimu, Mamalishe, Wajumbe wa Baraza Kuu la Kina mama, Maafisa Ugani na Watendaji wa Kata.

Aidha, kupitia Kongamano hilo, Waziri Ulega alimshukuru Mhe, Rais, Dkt. Samia kwa kumuongezea mitungi hiyo 500, huku akisema hatua hiyo inaonesha wazi dhamira yake ya kuwanusuru wakina mama na matumizi ya kuni na mkaa.

Naye, Mgeni Rasmi wa Kongamano hilo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wenye Mahitaji Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amempongeza  Mbunge na Uongozi wa Wilaya ya Mkuranga kwa hatua hiyo ya kuwawezesha kina mama nishati safi ya kupikia kwani ni njia moja wapo ya kuwakwamua kina mama hao kiuchumi.

Itakumbukwa kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa nchini Dubai katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP 28), pia alizindua Mradi wa Nishati Safi ya kupikia kwa lengo la kuwasaidia Wanawake Barani Afrika (AWCCSP).