
Kesi ya unyanyasaji, iliyokuwa ikimkabili Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Pauline Gekul, dhidi ya Mfanyakazi wake Hashim Ally, imefutiliwa mbali.
.
Hakimu Mkazi wa mahakama ya Wilaya ya Babati, Victor Kimario, amesema uamuzi huo umefuata baada ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kuona hana nia ya kuendelea na kesi hiyo, na kwamba ameiondoa kwa mujibu wa kifungu cha 91 (1), cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022 ambayo inampa DPP Mamlaka ya kuondoa kesi yoyote ya jinai Mahakamani kabla haijafikia hukumu na bila kutoa sababu za uamuzi huo.
.
Kulingana na hati ya malalamiko ya kesi hiyo, Mbunge huyo alikuwa akikabiliwa na shtaka moja shambulio na kusababisha madhara kwa mwili chini ya kifungu cha 241 cha sheria ya kanuni ya adhabu, sura ya 16, marekebisho ya mwaka 2022.
.
Inadaiwa kuwa Mbunge huyo na watu wengine ambao hawapo katika malalamiko hayo, Novemba 11, 2023, mjini Babati, mkoani Manyara walimuita Hashim na kumuweka kizuizini ambapo walimtishia kwa silaha ya moto, kisha kumvua nguo na kumlazimisha kukalia chupa ya soda ili iingie katika sehemu yake haja kubwa.
.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Wakili wa upande wa Mlalamikaji, Peter Madeleka amesema wanakusudia kukata rufaa kwa kuwa hawajaridhishwa na maamuzi yaliyotolewa na Mahakama.
