Back to top

PINDA AKAGUA ENEO WATAKALOHAMISHIWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO HANANG

05 January 2024
Share


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Geophrey Pinda, ametembelea na kukagua eneo ambalo limepimwa viwanja kwa ajili ya kuwahamisha waathirika wa mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang.

Mhe.Pinda amefanya ukaguzi huo leo akiambatana na mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga pamoja na viongozi wengine wa mkoa pamoja na wa wilaya ya Hanang.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imeshiriki pamoja na na wadau wengine katika zoezi la kutathmini kiwango cha uharibifu uliotokana na maafa yaliyotokea tarehe 3 Desemba 2023 na kushauri juu ya maeneo yanayoweza kutumika kuhamisha waathirika.

Akiwa katika eneo hilo wilayani Hanang mkoani Manyara, Mhe.Pinda alielezwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Manyara, Wenceslaus Mtui kuwa, jumla ya ekari 100 kutoka Jeshi la Magereza kwenye eneo la Warret zimetolewa kwa ajili ya waathirika.

Tarehe 21 Desemba 2023 Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenister Mhagama alielekeza wizara ya Ardhi kuhakikisha viwanja kwa ajili ya kuhamisha waarhirika maeneo ya Gendavi, Jorodom, Ganana na Katesh - Hanang vinapimwa na kukamilika kabla ya Des 31. 2023

Kwa mujibu wa Mtui, zoezi la upimaji viwanja katika eneo hilo lililotolewa na Jeshi la Magereza umefanyika kwa weledi na kukamilika ndani ya siku saba ambapo jumla ya viwanja 269 vilipimwa na kupandwa mawe.

Amesema, viwanja vilivyopimwa viko katika mgawanyo wa makazi 226, makazi na biashara 26, pamoja na  huduma za jamii 17.  Hata hivyo, suala la uandaaji hati linasubiri maelekezo pamoja na orodha rasmi iliyohakikiwa na kuidhinishwa na mamlaka husika. 

Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ameishukuru Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kufanya kazi kubwa ya kupima viwanja na kuweka mawe katika kipindi cha muda mfupi.

Kwa upande wake Naibu Waziri Pinda amesema, wizara yake imeshafanya jukumu lake la msingi la kupima eneo hilo na kutoa wito kwa TARURA kuharakisha uchongaji barabara kuelekea eneo hilo ili kurahisisha usafirishaji vifaa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hanang Rose Kamili ameishukuru wizara ya ardhi kwa kazi nzuri ya upimaji eneo wanalohamishiwa waathirika wa mafuriko ya maporomoko ya tope na mawe

Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang yamesababisha jumla ya wananchi 87 miili yao kupatikana baada ya kupoteza maisha na majeruhi kuendelea kupata matibabu katika hospitali ya Hydom, wilaya na mkoa.Sambamba na hilo baadhi ya wananchi wanaendelea kupata hifadhi katika maeneo ya taasisisi za elimu zilizopo Katesh baada ya makazi yao kuharibiwa.