
Wizara ya Katiba na Sheria imesema imejipanga kikamilifu kuhakikisha Wananchi wote wananufaika na Kampeni ya Mama Samia Legal Aid ambayo imelenga kutoa msaada wa kisheria bure kwa jamii katika masuala ya migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi na matunzo ya Watoto.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pindi Chana amesema hayo alipozungumza na Wananchi na kuzindua kampeni hiyo
katika Viwanja vya Stendi ya zamani Mkoani Singida, leo tarehe 10 Januari 2024; ambapo ameeleza kuwa msaada wa kisheria unatolewa bure katika Halmashauri zote za Mkoa wa Singida kuanzia kesho tarehe 11 Januari 2024 hadi tarehe 19 Januari, 2024.
Amesema malengo ni kufikia jumla ya Kata 70 na vijiji 210 vya mkoa wa Singida; hivyo ametoa Wito kwa Wananchi wote wa Mkoa huo na maeneo jirani kuitumia vizuri fursa hiyo kwa kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu kwa kupata elimu na huduma za masuala mbalimbali ya kisheria zitakazotolewa bure na kuwataka viongozi katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalamu wetu watakapokuwa katika maeneo yao wawahamasishe wananchi wajitokeze kwa wingi kupata huduma hiyo.
Amesema Mama Samia Legal Aid Campaign imefikia mikoa mitano (05) ya Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma na Simiyu ambapo jumla Halmashauri 35, Kata 397 na Vijiji/ Mitaa 1,046 imefikiwa katika utekelezaji wa Kampeni hiyo na Katika mikoa hiyo mitano, jumla ya wananchi 362,488 (Wanaume 179,874 wananwake 182,615) wamefikiwa kupitia elimu ya kisheria na huduma nyingine za kisheria.
Ameongeza kuwa kampeni hiyo imeshiriki katika utatuzi wa migogoro katika ngazi za kijamii, jumla ya migogoro 6,365 iliyohusu masuala ya ardhi, ndoa, mirathi na matunzo ya watoto ilipokelewa ambapo kati ya hiyo migogoro 488 ilitatuliwa na kuhitimishwa katika kipindi cha Kampeni. Migogoro 5,877 inaendelea kushughulikiwa katika mamlaka mbalimbali za kimahakama na kiutawala na Wizara kupitia waratibu na wasajili wa mikoa na wilaya imeendelea kufuatilia utekelezaji wake.
