
Wananchi 15,000 kutoka Halmashauri saba za Mkoa wa Singida wamefikiwa na huduma ya msaada wa Kisheria bure, inayotolewa na Kampeni ya Mama Samia Legal Aid, inayoendelea kutekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria Mkoani humo mpaka tarehe 19 Januari 2024.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria ambaye pia ni Msajili wa Mashirika yanayotoa huduma za Msaada wa Kisheria Tanzania, kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi.Ester Msambazi amesema mwitikio wa Wananchi ni mkubwa sana tofauti na walivyokuwa wanahofia kutokana na ni msimu wa mvua labda Wananchi watakuwa Mashambani, lakini wamejitokeza kwa wingi sana kupata huduma za msaada wa kisheria katika kila Halmashauri ambapo timu ya kampeni hiyo inafanya kazi.
Amesema Mpaka sasa ana uhakika kwamba Wizara ya Katiba na Sheria inaenda kuvuka lengo kwa maana ya idadi ya Wananchi ambao walikuwa tarajia kuwafikia imekuwa ni kubwa zaidi ya matarajio, kwani kila Halmashauri wanatarajia kwenda kata 10 kwa hiyo kwa Mkoa wa Singida watakuwa wameenda kata 70 na Vijiji zaidi ya 210, pia watakwenda kwenye vituo vya Polisi vya kila Wilaya na katika Magereza yote za Mkoa wa Singida ili kuwasaidia wale ambao wapo ndani ambao hawawezi kutoka na kuja kupata huduma hii ya msaada wa kisheria.
Bi.Ester ameeleza kuwa kampeni hiyo imeimarisha mahusiano baina ya Serikali na wadau wengine ambao ni watoa huduma za Kisheria na kwamba ushirikiano ni mkubwa sana baina ya Taasisi hizo katika ngazi zote, ikiwemo Watendaji wa Vijiji na Vitongoji ambao nao wamejengewa uwezo na kukumbushwa kuhusu wajibu wao na matarajio ni kwamba kila Mwananchi atapata usaidizi wa kisheria popote pale alipo.
Aidha Takwimu za awali za kampeni hiyo zinaonesha kuwa migogoro mikubwa iliyopo ni ile inayohusisha matumizi ya Ardhi inaongoza ikifuatiwa na migogoro ya Ndoa na matunzo ya Watoto.
