
Chama cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali ibadili utaratibu wa ununuzi wa mazao ya wakulima kwa kuweka mfumo wa malipo ya papo kwa papo ili kuwapa matumaini zaidi wakulima nchini.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Mhe.Othman Masoud Othman, ametoa wito huo alipozungumza na wafuasi wa chama hicho katika viwanja vya Mingayo, Mnazi Mmoja mkoani Lindi.
Amesema utaratibu wa sasa wa serikali kununua mazao ya wakulima kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, hauwapi matumaini wakulima kwa kuwa inachukua muda mrefu kwa wakulima kusubiri malipo yao jambo linaleta kero kwa wananchi na linapaswa kuondoka.
Amesema serikali haipaswi kuendelea kununua mazao ya wakulima kwa mtindo huo wa stakabadhi ghalani, badala yake iandae malipo mara wakulima wanapopeleka na kuuza mazao yao katika masoko mbali mbali nchini.
