Back to top

MSHAURI ANG'OLEWA, TANROADS WAPEWA JUKUMU

25 January 2024
Share

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameagiza kuondolewa kwa Mhandisi Mshauri LEA Associaties anayesimamia ujenzi wa barabara ya Kitai - Lituhi sehemu ya Amani Makoro-Ruanda kwa kiwango cha lami na kuutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuendelea kusimamia ujenzi huo ili uweze kukamilika.

Pia, ameagiza Mkandarasi anayejenga barabara hiyo China Railway Seventh Group kutopewa miradi mipya mpaka hapo atakapokamilisha miradi aliyopewa katika mkoa wa Mara, Katavi ambayo nayo inaonekana kusuasua.

Bashungwa ametoa agizo hilo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wakati akikagua ujenzi wa barabara hiyo ambapo hajaridhishwa na utekelezaji wake ambao umechelewa kwa asilimia 75 na kusisitiza hatua za kimkataba zichukuliwe dhidi ya Mhandisi Mshauri huyo.

Bashungwa ameagiza TANROADS kutoendelea kulimbikiza miradi kwa Wakandarasi kwani ndiyo inafanya miradi mingi kuchelewa  na mingine ikiwa ya kimkakati na kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Jephason Nko, amesema kuwa maendeleo ya mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 25 ikilinganishwa na asilimia 100 ambapo mradi huo ulitakiwa kukamilika  Disemba, 2023.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma , Kanali Labani Thomas, amesema kuwa Mchuchuma na Liganga wanaitegemea barabara hii kwani ndio barabara muhimu na ni kiunganishi cha kutoka Mkoa wa Ruvuma kupitia Nyasa kwenda mkoani Njombe  kupitia Ludewa.

Waziri Bashungwa yupo mkoani Ruvuma katika ziara yake ya kikazi ambapo atakagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara na madaraja.