Back to top

DARAJA LA ZEGE SULUHU KWA WAKAZI MITOMONI -RUVUMA.

26 January 2024
Share

Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) wamepewa miezi miwili kufanya usanifu wa kina na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa daraja la zege, katika eneo la Mitomoni mkoani Ruvuma, ili wananchi wa maeneo hayo, waondokane na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma mbalimbali za kijamii.

Agizo Hilo limetolewa na Waziri wa Ujenzi Mhe.Innocent Bashungwa, katika ukaguzi wa miundombinu ya barabara kutokea Songea Mjini hadi kufika Wilaya ya Nyasa kupitia barabara ya Likuyufusi - Mtomoni.

Waziri Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo utaunganishwa na barabara ya Unyoni Mpapa - Liparamba - Mkenda pamoja na barabara ya Likuyufusi - Mkenda kupitia Mto Ruvuma.

Naye Mkazi wa eneo hilo, Hadija Manyama, ameeleza kuwa wanapata shida ya usafiri na usafirishaji wa mazao yao upande wa pili hadi kufikia kuuza kwa bei ya hasara kwa sababu hakuna daraja la kuvuka.

Kutokana na changamoto ya miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo hayo, Waziri Bashungwa amelazimika kutumia takribani saa tano kwa kutumia usafiri wa miguu, mitumbwi na pikipiki maarufu kama bodaboda hadi kufikia vijiji hivyo.