Back to top

PAC: OSHA WASHIRIKISHWE MANUNUZI SERIKALINI

26 January 2024
Share

Serikali imeshauriwa kuutumia Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), kuainisha viwango vya usalama na afya katika samani na vifaa mbalimbali vya ofisi kabla ya manunuzi kufanyika ili kuepuka kununua samani na vifaa visivyokidhi viwango stahiki na kusababisha madhara kwa Watumishi wa umma.
.
Ushauri huo umetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), baada ya Kamati hiyo kupewa mafunzo kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, yaliyotolewa na wataalamu wa OSHA, yaliyoongozwa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda.


Aidha Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, amesema kupitia mafunzo hayo wamebaini kuwa samani na vifaa mbali mbali visivyozingatia viwango vya usalama na afya vimeendelea kununuliwa katika majengo na ofisi za serikali licha ya kuwepo kwa Taasisi ya OSHA ambayo ingeweza kutoa ushauri juu ya viwango stahiki.
.
Pia, Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa OSHA inapaswa kushirikishwa kikamilifu katika miradi ya ujenzi wa majengo ya serikali hususan katika Mji wa Serikali unaoendelea
kujengwa katika eneo la Mtumba Jijini Dodoma ili ujenzi huo uweze kuzingatia uwepo wa miundombinu rafiki kwa ajili ya kulinda afya na usalama wa watumishi wa umma na
wananchi kwa ujumla.