Back to top

WATAALAMU ELIMU MAALUMU WAPEWA MAFUNZO MTAALA ULIOBORESHWA

28 January 2024
Share

Serikali imesema inaendelea na jitihada za kuhakikisha watekelezaji wote wa mitaala wanapata uelewa wa maboresho yaliyofanyika katika mitaala hiyo, ambapo katika kutekeleza jitihada hizo imetoa fedha kwa ajili ya mafunzo kwa maafisa elimu maalumu wa Halmashauri zote nchini.


Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Prof. Maulid Mwatawala, leo Januari 27, 2024, wakati akifungua mafunzo ya uwezeshaji wa maafisa elimu maalumu wa Halmashauri kuhusu usimamizi wa utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa, mkoani Morogoro.
.


"Katika kuendelea kuhakikisha kuwa watekelezaji wote wa mitaala wanapata uelewa wa maboresho yaliyofanyika katika mitaala, sasa serikali imetoa fedha kwa ajili ya  mafunzo kwa Maafisa Elimu Maalumu wa Halmashauri zote nchini." Alisema Prof.Mwatawala.


.
Aidha, Prof.Mwatawala amewataka washiriki wote wa mafunzo hayo kuhakikisha wanashiriki vema katika mafunzo ili wakasimamie vema na kuimarisha usimamizi wa ujifunzaji na ufundishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Dkt. Aneth Komba amesema utoaji wa mafunzo haya umefanyika kufuatia kukamilika kwa mafunzo ya jumla ya utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa ya Elimu ya Awali na Msingi ya mwaka 2023.
.
Katika hatua nyingine, Dkt. Komba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa za kutosha zilizowezesha mafunzo haya, huku akiishukuru Wizara ya Elimu kwa kuendelea kutafuta fedha kwaajili ya mafunzo ya Mtaala ulioboreshwa kwa walimu wenye mahitaji maalumu.