
Waziri wa Ujenzi, Mh. Innocent Bashungwa amemuagiza Mkandarasi Vikosi vya Ujenzi, kuongeza umakini na kasi katika ujenzi wa jengo la Wizara hiyo linalojengwa katika Ofisi za Serikali Mtumba, jijini Dodoma ili liwe jengo la mfano na lenye utofauti.
Bashungwa ametoa agizo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo ambalo hivi sasa limefikia asilimia 71 na kusisitiza ubora na viwango katika utekelezaji wake.
Bashungwa amemsisitiza Mkandarasi huyo kutekeleza hatua za mwisho za ujenzi vizuri (finishing) ili Ofisi hiyo kuwa ya mfano, sambamba na kuwa na mkakati wa kuwapa maarifa wataalamu wa Sekta ya Ujenzi ili kuwawezesha wataalamu hao kupata ujuzi na kuweza kutekeleza kazi hizo wenyewe.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Vikosi vya Ujenzi, Mhandisi Simeoni Machibya, amemhakikishia Waziri huyo kuwa ujenzi wa jengo hilo utazingatia viwango na ubora ili kufikia malengo ya Serikali.
