
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Lazaro Twange amesema wananchi wa maeneo ya Mbagala na viunga vyake sasa wanatarajia kupata umeme wa uhakika baada ya Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mbagala kuongezewa uwezo kutoka Megawati 45 za awali na kufikia Megawati 165.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea Kituo hicho Bw. Twange alisema kuwa Kituo hicho kimeongezewa uwezo mara mbili ya awali hivyo kitakuwa na uwezo mkubwa wa kusambaza umeme na kuondoa kabisa changamoto ya kukatika kwa umeme katika maeneo hayo.
“Kituo hiki kimeongezewa uwezo mara mbili ya awali na mpaka sasa utekelezaji wa Mradi huu umefikia asilimia 70. Wananchi wa Mbagala na viunga vyake sasa wategemee umeme wa uhakika’’ alisisitiza Bw. Twange.
Pia, Mkurugenzi Mtendaji Bw. Lazaro amemshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa kiasi cha fedha Dola za Kimarekani milioni 6.4 ili kufanikisha Mradi huu wenye tija na manufaa kwa wananchi wa maeneo hayo na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sixtus Mapunda, akizungumza wakati wa ziara hiyo amepongeza jitihada zinazofanywa na TANESCO ambapo amefafanua kuwa kukamilika kwa Mradi huo kutasaidia kumaliza kero ya umeme katika maeneo mengi ya Mbagala, Temeke na Mkuranga.
“Kwa namna ya pekee tunaishukuru sana TANESCO kwa mradi huu, kwa awamu ya kwanza Mradi huu ulipaswa kujaribiwa mwezi Juni mwaka huu lakini Mradi umeweza kuonesha mafanikio kabla ya wakati kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa’’ alifafanua Mhe. Mapunda
Uboreshaji wa Mradi huu wa Kituo cha Kupokea na Kupoza na Kusambaza umeme cha Mbagala umegharimu Dola za Kimarekani milioni 6.4 ambapo sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji wake na kukamilika kwake kunatarajia kusambaza umeme wa Megawati 165.