
Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu , amesema tangu ugonjwa wa Marburg ulipogundulika mkoani Kagera, watu waliopata maambukizi walikuwa ni 9 kati yao 3 wamepona na 6 walifariki dunia, akiwemo mtumishi mmoja wa afya na mtoto mwenye umri wa miezi 18.
Amesema wagonjwa wawili wa Marburg waliokuwa wamesalia katika vituo maalumu vya matibabu, waliruhusiwa kutoka tarehe 20 na 21 Aprili 2023 ,baada ya kuthibitika kimaabara kwamba hawana virusi vya MARBURG.
Akiongea na Wanahabari, Waziri Ummy ,amesema kuanzia tarehe 21 Aprili 2023, hadi leo hakuna mgonjwa yeyote mwenye virusi vya Marburg Mkoani Kagera.
Aidha Waziri Ummy amebainisha kuwa, serikali itaendelea na ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa wa Marburg, na endapo hakutatokea mgonjwa mpya baada ya siku 42 yaani ifikikapo 31 Mei 2023, serikali itatangaza rasmi kumalizika kwa ugonjwa huo nchini.
Ameongeza kuwa, kutokana na ushirikiano wa pamoja na wananchi, wadau na serikali, umefanikisha kudhibiti ugonjwa huo wa MARBURG.


