Back to top

AHUKUMIWA MAISHA JELA KWA KUMLAWITI MTOTO (6).

09 June 2023
Share

Mahakama ya Wilaya ya Rufiji imemhukumu kifungo cha maisha gerezani, Shabani Hassani Njechele (32) Mkazi wa Mohoro baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 6.

Njechele ambaye ni Mkazi wa eneo la Mohoro Magharibi Wilayani Rufiji Mkoani Pwani amehukumiwa adhabu hiyo Juni 8, 2023 na Hakimu Mkazi Flora Bernard Mujaya baada ya kumtia hatiani kwa kosa hilo la kumlawiti mtoto kwa nyakati tofauti akiwa nyumbani kwake (Mtuhumiwa).

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mujaya amesema mahakama imemtia hatiani Mtuhumiwa aliyekuwa anakabiliwa na kosa la ulawiti kinyume na kifungu cha 154(1)(a) cha sheria ya kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Amesema katika kesi hiyo ya jinai namba 192/2022 upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha kosa hilo pasipo na shaka kupitia mashahidi wake watano.

Awali, wakili wa Serikali Justine Sanga ameiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine hasa ukizingatia kitendo alichokifanya kwa mtoto umri mdogo wa miaka 6.