Back to top

AIRTEL AFRIKA KAMPUNI YA KWANZA KUZINDUA HUDUMA YA STARLINK MOBILE DRC

15 August 2026
Share

Airtel Africa imeandika historia baada ya kuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano barani Afrika kuzindua huduma ya Starlink Mobile nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ikifungua ukurasa mpya katika upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo yasiyofikiwa na minara ya kawaida ya simu.

‎Huduma ya Starlink Mobile, iliyozinduliwa kwa ushirikiano kati ya Airtel Africa na Starlink, inawezesha wateja wenye simu janja kupata huduma za mawasiliano katika maeneo yasiyo na miundombinu ya kawaida ya mawasiliano.

‎Starlink ina zaidi ya satelaiti 650 zinazosaidia huduma za kunasa mawimbi ya mawasiliano kwenye simu (satellite-to-mobile) duniani. Kwa sasa, huduma ya satelaiti inalenga programu zinazotumia kiwango kidogo cha data za intaneti, zikiwemo ujumbe wa WhatsApp na SMS, bila kuhitaji wateja kuwa na vifaa maalum au kifaa cha ziada.

‎Uzinduzi huo unafuatia makubaliano ya kimkakati yaliyotangazwa na Airtel Africa na Starlink mwezi Desemba 2025, pamoja na majaribio ya huduma za data na SMS nchini Kenya mwezi Machi 2026.

‎DRC imekuwa soko la kwanza la Airtel Africa na nchi ya kwanza barani Afrika ambako Starlink Mobile imefika.

‎Akizungumza kuhusu uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kupanua mawasiliano barani Afrika.

‎“Uzinduzi wa kwanza kabisa wa kibiashara wa Starlink Mobile barani Afrika ni hatua kubwa kwa Airtel Africa kupitia ushirikiano wetu na SpaceX. Kwa kuchanganya mtandao wa ardhini (minara) wa Airtel na teknolojia ya satelaiti ya Starlink, tunapanua mawasiliano ziaidi ya mipaka ya miundombinu ya kawaida ya simu za mkononi,” alisema Taldar.

‎Alisema uzoefu unaopatikana DRC utasaidia Airtel Africa katika kupanua huduma hiyo ya satelaiti kwenye masoko mengine ya kampuni, kwa kuzingatia idhini za mamlaka za udhibiti katika kila nchi.

‎Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Airtel DRC, Thierry Diasnoma, alisema huduma hiyo ya satelaiti itaongeza fursa za mawasiliano katika nchi yenye eneo kubwa kijiografia na ambako baadhi ya wananchi wanaishi au kufanya kazi mbali na miundombinu ya kawaida ya mawasiliano.

‎“Huduma hii inatoa safu ya ziada ya mawasiliano, ikisaidia wateja kuwa mtandaoni muda wote, wakipata taarifa na kuunganishwa katika maeneo ambayo mtandao wa minara haupatikani,” alisema Diasnoma.

‎Huduma hiyo inalenga pia kuwasaidia wasafirishaji na kampuni za usafirishaji na usambazaji, mashirika ya yasiyo ya kiserikali, wafanyakazi wa afya, wakulima, kampuni za uchimbaji madini na jamii zinazoishi katika maeneo ambayo hayajafikiwa kikamilifu na mitandao ya ardhini.

‎Aidha, teknolojia hiyo inaweza kuwa nyenzo muhimu katika mawasiliano ya dharura wakati wa majanga ya asili au pale ambapo mtandao wa kawaida unakatika kwa muda.

‎Kwa sasa, wateja wanaotaka kutumia huduma hiyo wanapaswa kuwa na simu janja ya Android yenye LTE inayooana na mfumo wa Starlink Mobile, pamoja na kifurushi cha data cha Airtel DRC kinachokidhi vigezo au huduma ya data roaming iliyowashwa.

‎Airtel imesema vifaa vya Apple vitaanza kusaidiwa katika siku zijazo.

‎Wateja wanaokidhi vigezo wanaweza kujisajili kupitia MyAirtel App na kupata huduma ya majaribio bila malipo kwa siku 30 za kwanza.

‎Baada ya kipindi hicho cha utambulisho, huduma itaendelea kupatikana kupitia vifurushi vya data vya Airtel vinavyokidhi masharti.

‎Airtel Africa na Starlink zimesema zinaendelea kuboresha huduma hiyo, huku uwezo wa ziada ukitarajiwa kuongezwa kadri teknolojia inavyoendelea kukua na idhini za udhibiti zinavyopatikana.

‎Uzinduzi huo unaiweka Airtel Africa katika nafasi ya kampuni ya kwanza ya mawasiliano barani Afrika kuanza kutoa huduma ya satelaiti katika simu, huku ikiendelea kutumia teknolojia mpya kupanua wigo wa mawasiliano na kuongeza ujumuishwaji wa kidijitali barani Afrika.