
Wakati Jeshi la Polisi mkoani Songwe, likiendelea na oparesheni, misako pamoja na doria katika maeneo mbalimbali limefanikiwa kukamata silaha mbili aina ya Bastola (Pistol) zote katika mji wa Tunduma, uliopo wilayani Momba, mkoani Songwe, ambapo moja ya bastola ambayo ni mpya imekutwa imetelekezwa kwenye maegesho ya magari eneo la Majengo, ikiwa ndani ya boksi lake pamoja na makasha matatu ya risasi zikiwa jumla mia moja na hamsini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, SACP. Augustino Senga, amesema uchunguzi wa awali umebaini silaha hiyo aina ya Retay G91c yenye namba R1YGCMOYO1-2400425 Cal. 9mm yenye rangi nyeusi iliyoingia nchini isivyo kihalali ambapo jeshi la polisi wanaendelea na msako mkali kumtafuta mtu au watu waliohusika na tukio hilo.
Kamanda senga maeongeza kuwa silaha nyingine ni aina ya CZ92 Browning, yenye namba A.428007, Caliber 6.35mm, ikiwa na risasi sita yenye rangi ya dhahabu na nyeusi iliyoibiwa eneo la Haloli, wilayani Mbozi, baada ya kutokea uvunjwaji wa nyumba ya Bw. Emmanuel Fungo, mmiliki halali wa silaha hiyo imekamatwa katika eneo la Soko la Black Tunduma, huku mtuhumiwa akifanikiwa kukimbia huku msako mkali ukiendelea.
Kkatika hatua nyingine Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, SACP Augustino Senga kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, amewatunuku vyeo mbalimbali maafisa sitini na mbili wa jeshi hilo baada ya kupata mbinu na mafunzo maalum ya kuvitumikia vyeo hivyo.
Akizungumza na askari hao makao Makuu ya Jeshi, hilo mkoani humo eneo la Vwawa Mbozi, waliopandishwa vyeo kwa ngazi za Koplo, Staff Sajent na Sajini Meja, Kamanda Senga kando na kuipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha jeshi hilo, amewataka kuwa wazalendo na kuhakikisha mbinu na mafunzo waliyopata vinakuwa msaada wa jamii.