Back to top

BIL. 9.88 KUJENGA LAMI DAREDA MJINI - DAREDA MISSION BABATI

06 April 2024
Share

Waziri wa Ujenzi Mh.Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara (TANROADS) kumsimamia Mkandarasi kampuni ya Jiangxi Geo Engineering kukamilisha kwa wakati ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Dareda hadi Dongobesh (km 60) sehemu ya kwanza ya Dareda Mjini hadi Dareda Missioni (km 7) ili kuufungua kiuchumi Mkoa wa Manyara.

Bashungwa amezungumza hayo Wilayani Babati Mkoani Manyara wakati akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) na kampuni ya M/s Jiangxi Geo Engineering (Group) Corporation ya China kwa gharama ya Shilingi Billioni 9.88. 

Bashungwa amemtaka Mkandarasi huyo kuhakikisha anakamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Labay-Haydom (km25) na barabara ya Mbulu-Garbabi (km 25) ambapo Serikali inakwenda kulipa madeni ambayo alikuwa anayadai ili miradi yote iweze kukamilishwa kwa haraka.

Aidha, Bashungwa amempongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kwa kutekeleza maagizo ya Wizara ya kutolimbikiza kazi nyingi kwa Mkandarasi mmoja na hivyo miradi mingi kuchelewa na kusababishia hasara Serikali.

“Nikupongeze Mtendaji Mkuu kwa kutumia hatua za kimkataba kumuondoa Mkandarasi wa barabara ya Lukuyufusi - Mkenda Mkoani Ruvuma mara baada ya kuona hafanyi vizuri kwenye maeneo mengine”. Bashungwa.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendinga amesema mradi huu unapita katika Wilaya ya Mbulu na Babati na ujenzi wa barabara hii inakwenda kuongeza thamani ya mazao ya shamba ikiwemo kilimo na ufugaji pia itarahisisha wananchi kufanya biashara pembezoni mwa barabara na kukuza uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Mkoa kwa ujumla.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amesema kuwa zabuni kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya pili ya Dareda Mission – Dongobesh  inatarajiwa kutangazwa katika Mwaka huu wa fedha 2023/24.