
Wadau mbalimbali wametakiwa kuendelea kutoa elimu mashuleni kwa watoto juu ya namna ya kujikinga dhidi ya vitendo vya ukatili na kuhakikisha wanatoa taarifa pale wanapohisi kutaka kufanyiwa ukatili au wanapofanyiwa ukatili ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Athuman Katimba, jijini Dodoma alipokuwa akifungua kikao cha robo ya kwanza cha wadau wanaotekeleza afua za eneo namba tano la MTAKUWWA linalohusika na usimamizi wa utekelezaji wa Sheria.
Mhe. Katimba amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na wadau wote katika jitihada za kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili havina nafasi katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
“Jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau wote zimeendelea kuleta matokeo chanya katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, hata hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu ikiwemo Serikali, wadau na wananchi kwa ujumla kuhakikisha tunaimarisha zaidi uratibu, ubunifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kutokomeza ukatili” alisema Mhe. Katimba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Huduma za Msaada wa Kisheria, Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Ester Msambazi alisema kuwa lengo la kikao hiki ni kuhakikisha mikakati ya pamoja ya kumuhudumia mwananchi inawekwa.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkaazi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Bw. Evance Mori, alisema wadau wa maendeleo wako tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mifumo inaimarishwa na ukatili unatokomezwa.
