
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Mhe. Subira Mgalu, amekabidhi magari mapya kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika kuwahudumia Wateja wilayani Bagamoyo.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Ofisi ya TANESCO Bagamoyo, Mhe. Mgalu amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme kwa wakati, kwa ubora na kwa uhakika zaidi.
“Magari haya yatawezesha mafundi na wahandisi wa TANESCO kuwafikia wananchi kwa haraka pale panapotokea hitilafu au changamoto za umeme. Tunataka kuona muda wa kushughulikia matatizo unapungua na huduma inaboreshwa,” amesema Mhe. Mgalu.
Amesisitiza kuwa, hivi sasa TANESCO imeimarika katika utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na kutoka katika kutengeneza hasara na linajiendesha bila kupata ruzuku kutoka Serikalini.
Aidha, amesema baada ya kukamilika bwawa la Julius Nyerere linalozalisha megawati 2115 na kupelekea Nchi kuwa na uwezo wa takribani wa megawati 4,000 huku mahitaji yakiwa takribani megawati 2,000 hivyo kuitaka TANESCO kuongeza kasi ya kuwaunganishia wateja.
Mkurugenzi wa TANESCO Kanda ya Mashariki,Mha. Kenneth Boymanda amesema TANESCO inatekeleza miradi mingi ya maendeleo Wilaya ya Bagamoyo ikiwemo ya umeme Vijijini hivyo upatikanaji wa magari hayo kutarahisisha utekelezaji wa miradi hiyo.
“Bagamoyo tunao mpango mkubwa wa kuhakikisha kila nyumba inafikishiwa nishati ya umeme nak ama Nchi mpaka mwaka 2030 kuunganisha nyumba milioni nane na laki tatu na nyumba Milioni Moja na Laki Saba kwa mwaka”, amesema Mha. Boymanda
Ameongeza kuwa, majukumu hayo yanahitaji uwepo wa vitendea kazi na kusisitiza kuwa TANESCO itafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Serikali kupitia mpango wa mission 300.
Serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuboresha miundombinu ya umemme kama msingi wa maendeleo ya viwanda, biashara na ustawi wa jamii.
Hatua ya TANESCO kununua magari hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma kwa wateja na kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.
