Back to top

ENEO LA KITARAKA KUTUMIKA KIMKAKATI KUZALISHA MIFUGO KIBIASHARA

31 January 2023
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega, amesema Serikali imedhamiria kulitumia eneo la kupumzishia mifugo la Kitaraka lililopo wilayani Manyoni, Singida liweze kutumiwa na vijana watakao hitimu mafunzo katika vituo atamizi, kwa ajili ya kufanya shughuli za uzalishaji wa mifugo kibiashara ili kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Mhe.Ulega amebainisha hayo wakati wa kikao baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Singida, alipokutana nae katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida.

Wakati wa mazungumzo yao, Mhe.Ulega alimueleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa lengo la ziara yake ni kujadiliana nae kuhusu dhamira ya Serikali ya kutaka kulitumia eneo la kitaraka kwa ajili ya kufanya shughuli za uzalishaji wa mifugo ili kuwawezesha vijana  kujipatia ajira lakini pia kuzalisha malighafi ya uhakika kwa ajili ya viwanda vya nyama na kuifanya sekta ya mifugo  kuchangia ipasavyo katika pato la taifa na la mtu mmoja mmoja.

Amesema kuwa kupitia programu ya vituo atamizi iliyoanzishwa na serikali kwa ajili ya kuwafundisha vijana ufugaji wa kisasa, Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kufuga kibiashara kwa ajili ya kuuza  ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa mpango huo wa kutumia eneo la Kitaraka unatarajiwa kuzalisha robota 500,000 za malisho ya mifugo na kunenepesha ng’ombe 8000 kwa wakati mmoja.

Ulega amefafanua kuwa eneo hilo la Kitaraka limekaa kimkakati kwa ajili ya unenepeshaji wa mifugo kwasababu ndani ya eneo hilo kuna kituo cha treni ya mwendokasi (SGR) hivyo itarahisisha usafirishaji wa malighafi kutoka hapo kwenda maeneo mengine ya soko.

Aidha, Naibu Waziri alimuomba Mkuu wa Mkoa, uongozi wa halmashauri, na wananchi wa Singida kwa ujumla kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa dhati  katika kufanikisha adhma ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta ya mifugo.

“Serikali ya Mhe Rais, Dkt. Samia imejielekeza ipasavyo ktk kutumia fursa za sekta za Mifugo,uvuvi na kilimo katika kuajiri Vijana na kuongeza uzalishaji nchini hivyo naomba mtoe ushirikiano wa kutosha ili adhma hii iweze kutimia kama ilivyokusudiwa”,Mhe.Ulega