
Serikali imesema imeweka mazingira ya kuwawezesha vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali, kujitolea katika Taasisi za Umma kwa lengo la kuwawezesha kujipatia sifa za ziada zitakazowawezesha katika ushindani pindi nafasi mbalimbali zinapotangazwa.
Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma, katika kipindi cha maswali na majibu, na Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete, wakati akijibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Kamani Mbunge wa Viti Maalum, ambaye ameuliza kuwa Serikali haioni umuhimu wa kutoa kipaumbele cha ajira kwa Vijana wanaojitolea kutumikia Taifa, katika kada mbalimbali za Utumishi pindi nafasi za ajira zinapotolewa.
Katika majibu yake bungeni hapo Mheshimiwa Naibu Waziri Mhe. Ridhiwani Kikwete, ametumia wasaa huo kuwashauri na kuwahamasisha vijana wanaojitolea katika kada mbalimbali za Utumishi, wenye sifa stahiki kuomba nafasi za kazi pindi zitakapotangazwa ili waweze kushindana na waombaji wengine wenye sifa.
