Back to top

HATUA ZA MAKUSUDI ZICHUKULIWE KUSIMAMIA LISHE

30 September 2022
Share

Rais Samia Suluhu Hassan, ameagiza hatua za dhati na za makusudi zichukuliwe kusimamia sula la lishe, kwa kufuata mpango wa taifa wa chakula na lishe ili kujenga taifa lenye watu wenye afya njema kwa kufuta utapiamlo.

Akihutubia kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa usimamizi shughuli za lishe, Jijini Dodoma amesema changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa watu kuhusu lishe bora kuanzia ngazi ya taifa hadi kwenye familia.

Amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu sahihi ya lishe, ili kuepuka kuwa na rasilimali watu duni katika taifa kwa kuwa maendeleo yanapaswa kuwa ya watu na siyo ya vitu.

Aidha, amewaagiza Wakuu wa mikoa wahakikishe fedha zinazotengwa kwa ajili ya afua ya lishe zinatolewa kwa wakati na kufanya ufuatiliaji na tathimini ya utekelezaji wake na kuagiza TAMISEMI kuchukua hatua za nidhamu kwa waliotumia vibaya fedha hizo.