
Mahakama ya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, imemuhukumu kifungo cha maisha jela, Kijana aitwaye Hassan Hakika (18) baada ya kumpata na hatia ya kumlawiti mtoto mwenye ulemavu jina lake limehifadhiwa (15) ambaye alimlaghai na kisha kwenda naye kichakani ambako alimvua nguo na kumfanjia kitendo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kwa Waandishi wa Habari, Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Mtwara, SACP Issa J. Suleiman amesema tukio hilo limetokea Aprili 22, 2025 katika Kijiji cha Dinyeke.
Hukumu ya tukio imetolewa hivi karibuni mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Tandahimba Joseph Julius Waruku na mwendesha mashtaka Zuberi Ramadani Mngodo.
Katika hatua nyingine Mahakama ya wilaya ya Masasi imehukumiwa kwenda jela miaka 30 kila mmoja watu wengine watatu baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kulawati katika matukio tofauti.
Mahakama ya wilaya ya Masasi imemuhukumu Yujini Cleophane Venanti (56) mkazi wa Kijiji cha Mbonde wilayani humo kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kulawiti mwanaume mmoja (28) ambaye jina lake limehifadhiwa baada ya kumvizia mhanga akiwa jikoni anapika na kumsukuma kwa nguvu na kumuangusha kisha kumuingilia kinyume na maumbile.
Aidha Bakari Khamis Matole (21) mkazi wa kijiji cha Namakongwa amehukumiwa kwenda jela miaka 30 baada kumlaghai mwanafunzi wa kike (17) wa kidato cha nne.
Mwingine aliyehukumiwa ni Danfrod Boniphance Pota (32) mkazi wa Kijiji cha Namdenga baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 42, ambaye alimvamia kwa nguvu na kisha kutekeleza kitendo hicho.
Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashukuru wananchi kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwao huku likiwataka kutosita kutoa taarifa ya matukio yote ovu yanayoendelea kwenye jamii.