Back to top

KAMATI YA BUNGE YA AFYA YAKUTANA NHIF

22 September 2023
Share

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Stanslaus Nyongo leo jijini DSM imekutana na NHIF kujifunza na kupata taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake hususan maboresho yanayofanyika. 

"Tumekutana na NHIF leo, tumewasilikiza na tumewahoji mambo mbalimbali na tulichobaini hapa, wanafanya kazi kubwa pamoja na changamoto zilizopo hivyo yapo maelekezo ambayo tumewapa yakiwemo ya kuwafikia wananchi waliko ili kuwaelimisha na hatimaye wajiunge kwa wingi" alisema Mhe. Nyongo.

Kuhusu suala la uhai na uendelevu wa Mfuko, aliwatoa hofu wananchi juu ya taarifa hasi zinazotolewa kupitia vyombo mbalimbali hususan mitandao ya kijamii, taarifa ambazo zimekuwa zikileta hofu kwa wanachama na wananchi bila sababu ya msingi. 

"Mfuko huu haufi leo wala kesho, upo na unaendelea kutoa huduma hivyo niwatoe hofu na niwahamasishe kujiunga na huduma zake kwani ndio Mfuko pekee unaoleta uhakika wa matibabu," alisema Mhe. Nyongo.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alisema kuwa Mfuko umefarijika na ziara ya Kamati hiyo ambapo ameuhakikishia umma kuwa elimu itatolewa kwa ukubwa zaidi ili ifike kila mahali.

"Niwaombe sana wananchi waendelee kupokea elimu tutakapofika katika maeneo yao kwa ajili ili kila mmoja afahamu dhana ya Bima ya Afya na achukue hatua za kujiunga," alisema Bw. Konga. 

Kwa upande wa wajumbe wa Kamati hiyo, wote kwa pamoja waliupongeza Mfuko kwa jitihada kubwa zinazofanywa kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ubora na unafuu zaidi.