Back to top

KAMATI YAHIMIZA KASI UJENZI BANDARI YA UVUVI KILWA

16 March 2023
Share

Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imesema pamoja na hatua nzuri ya ujenzi wa bandari ya uvuvi iliyofikiwa, ni muhimu Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha kasi ya ujenzi huo, inaongezeka ili kutimiza adhma ya Mhe.Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuwa na bandari ya kwanza ya kisasa ya Uvuvi hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara Kilimo na Mifugo, Mhe.David Kihenzile wakati wa ziara ya kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi.

Mhe.Kihenzile amesema kuwa Serikali imetenga pesa za ujenzi  wa bandari hiyo kwa lengo la kuongeza kasi ya uvunaji wa rasilimali za uvuvi ili ziweze kusaidia kuinua uchumi na kuongeza fedha za kigeni ndani ya nchi.

Ameongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan  imedhamiria kutengeneza ajira Milioni 8  kwa ajili ya vijana kupitia Sekta za Kilimo, Mifugo na  Uvuvi, hivyo ujenzi wa bandari hiyo utakuwa ni sehemu ya majawabu ya upatikanaji wa ajira kwa vijana.

"Tumesisitiza kuwa kasi ya ujenzi iongezeke ili wananchi wanaosubiri waanze kunufaika na mradi huu", alisema Mhe. Kihenzile

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa wamepokea maelekezo, ushauri na maoni  ya kamati hiyo huku akisistiza kuwa kasi ya ujenzi wa bandari hiyo itaendelea kuwa kubwa zaidi ili waweze kutimiza  adhma ya Mhe. Rais,  Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na bandari ya uvuvi ya  kwanza na ya kihistoria hapa nchini.

Sambamba na hilo, Waziri Ulega ameitaka kampuni inayosimamia ujenzi wa Mradi huo ya China Harbour Engineering Company (CHEC) kuhakikisha inatoa fursa za ajira kwa vijana waliokaribu na mradi huo  ili na wao waweze kunufaika.

Ameongeza kwa kusema kuwa dhamira yao kama Serikali ni kuuendesha mradi huo kibiashara ili fursa nyingi za uwekezaji ziweze kupatikana na kwamba hapo mbeleni watatangaza fursa mbalimbali za uwekezaji hususani Viwanda ili kuchechemua uchumi wa Mkoa wa Lindi na nchi kwa ujumla wake. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa jumla ya Tsh. Bilioni 266.7 kwa ajili  ya Ujenzi wa mradi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko Mkoani Lindi ambao unatarajiwa kukamilika mwaka 2024.