Back to top

KAMPENI YA AFYA YA AKILI NI AFYA YAZINDULIWA

07 May 2025
Share

Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Bi. Ziada Sellah amezindua rasmi Kampeni ya kitaifa ya Afya ya Akili ni Afya, yenye lengo la kuongeza uelewa juu ya afya ya akili  nchini ili kuhakikisha kila mwananchi ana ustawi wa akili.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dodoma, katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, ambapo kampeni ya kitaifa ya "AFYA YA AKILI NI AFYA", ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Mwezi wa Uhamasishaji jamii juu ya uelewa wa Afya ya Akili (Mental Health Awareness Month) unaoadhimishwa mwezi Mei kila mwaka.

Bi. Ziada amesema Kampeni  hii inalenga kuhamasisha jamii nzima kuhusu umuhimu wa afya ya akili kama sehemu muhimu ya afya ya binadamu kwa ujumla.

“Kauli mbiu hii ina ujumbe mzito: “Afya ya akili ni afya”, hivyo hatuwezi kuwa na jamii yenye nguvu bila kuhakikisha kila mmoja ana ustawi wa akili, ”ameaema Bi. Ziada.

Amesema kuwa Afya ya akili ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya jamii na uchumi ambapo amesema bila afya ya akili iliyo imara, hakuna ufanisi kazini, hakuna furaha katika familia na hakuna mshikamano katika jamii.

Ameeleza kupitia kampeni hiyo, wanataka kuondoa unyanyapaa, kuhamasisha mazungumzo ya wazi kuhusu changamoto za afya ya akili na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora bila hofu wala unyanyapaa.

Tunaelewa kuwa changamoto za afya ya akili zinatokana na sababu mbalimbali za kibaiolojia, kisaikolojia, kijamii na kiuchumi, kwa mfano, umasikini, ukosefu wa ajira, magonjwa sugu, na majanga kama COVID-19 yameongeza kwa kiasi kikubwa mzigo wa changamoto za afya ya akili katika jamii yetu.

Ameongeza kuwa takwimu zinaonesha kuwa magonjwa kama sonona (depression), wasiwasi (anxiety) na utegemezi wa dawa za kulevya yanazidi kuongezeka, huku Shirika la Afya Duniani likikadiria kuwa mtu mmoja (1) kati ya wanne (4) duniani anakumbwa na tatizo la afya ya akili katika maisha yake.

Kupitia kampeni ya "AFYA YA AKILI NI AFYA", tunalenga kufikia malengo makuu manne ambayo ni Kuelimisha jamii kuhusu afya ya akili, dalili zake, na namna ya kupata msaada, Kupunguza unyanyapaa, Kuwezesha huduma bora za afya ya akili na Kushirikisha wadau wote

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuchukua hatua mahususi kuhakikisha huduma za afya ya akili zinaboreshwa.

"Tumeimarisha utoaji wa huduma katika hospitali za rufaa za mikoa na wilaya, na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ili kuwawezesha kutambua na kushughulikia masuala ya afya ya akili kwa ufanisi, "amefafanua na kuongeza kuwa tunapambana pia na changamoto za kifedha na unyanyapaa unaozuia watu wengi kufika vituoni kupata msaada.

Vile vile amesema pamoja na afua nyingine, kampeni hii ni jukwaa la kuunganisha nguvu. Tunatoa wito kwa waajiri, walimu, wazazi, walezi, viongozi wa dini, na vijana kote nchini kushiriki kikamilifu.

Amesema kuwa kila mmoja ana nafasi ya kuwa sehemu ya suluhisho iwe ni kwa kutoa msaada kwa rafiki mwenye changamoto, kusikiliza bila kuhukumu au kwa kushiriki katika shughuli za uelimishaji jamii.

“Aidha tukumbuke Afya ya akili ni afya na  hivyo hatuwezi kuwa na maendeleo ya kweli bila kuwekeza kwenye ustawi wa akili wa watu wetu. Hii ni kampeni ya kila mmoja wetu. Tuanze mwezi huu wa Mei kwa mabadiliko – mabadiliko ya fikra, vitendo, na sera,” amesisitiza Bi. Ziada.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Dkt. Paul Lawala amesema kampeni hiyo itafanyika kwa muda wa mwezi mmoja na ni jambo ambalo litakuwa endelevu kwa muda wa miaka mitatu.

“Ni harakati ya muda mrefu ya kuleta mabadiliko ya kifikra, kitabia na kimfumo kwa kushirikiana na vyombo vya habari, shule, sehemu za kazi, vituo vya huduma afya na viongozi wa jamii ili kuifikia jamii nzima kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikutano ya hadhara, vipindi vya redio na televisheni, mitandao ya kijamii na semina katika mashirika na taasisi mbalimbali,” amesema Dkt. Lawala.

Dkt. Lawala amesema kuwa kwa mwaka wa kwanza kampeni hiyo itafanyika katika mikoa ya Singida, Dodoma, Iringa, Morogoro na Manyara