Back to top

WAAJIRI WAAHIDI USHIRIKIANO NA PSSSF

19 November 2025
Share

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekutana na Maafisa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala pamoja na Maafisa Fedha (Wahasibu) katika vikao kazi vilivyofanyika mikoa ya Ruvuma na Kagera, lengo likiwa ni kuwaeleza maboresho yaliyofanywa na Mfuko na kuweka msisitizo wa matumizi ya huduma mtandao kupitia PSSSF Kidijitali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya vikao hivyo, wamesema hatua ya kuwafikia watumishi walio pembezoni mwa nchi ni nzuri na wameahidi ushirikiano ili kuhakikisha wanachama wanapata huduma bora na kwa wakati kwa mujibu wa sheria.

“ Mimi kama kiungo baina ya mtumishi na Mfuko kupitia PSSSF Kidijitali, nimeelezwa umuhimu wa kuwasilisha taarifa sahihi za mwanachama kwenye mfumo kuanzia anapojisajili siku anapoanza ajira, kwani itapelekea kuepuka usumbufu usio wa lazima na pia kuharakisha utoaji wa huduma.” Amesema Bi. Grace Mafuru kwa niaba ya washiriki wenzake.

PSSSF imeweka msisitizo kwa washiriki hao kuwa zaidi ya asilimia 95 ya huduma zake zinatolewa kupitia mtandao hivyo wametakiwa kuwajulisha watumishi kuchangamkia huduma hizo ili kuokoa muda na kupunguza gharama.

Huduma za Kidijitali zinamuwezesha mwanachama kujihudumia yeye mwenyewe na kupata huduma mbalimbali ikiwemo taarifa za michango yake, taarifa za mafao, kuwasilisha madai na kuuliza maswali mbalimbali akiwa mahali popote na kwa wakati wowote autakao. 

Kwa upande wake Meneja wa PSSSF Kanda ya Kusini, Bw. Sayi Lulyalya, amesema Maafisa hao ndio daraja au kiungo kati ya watumishi (wanachama) na Mfuko, kwani wanahusika katika michakato inayohusiana na uanachama wa mwanachama wa PSSSF tangu anapoajiriwa hadi anapostaafu utumishi wa Umma. 

Kwa hivyo Mfuko umeweka mkakati wa kuyafikia makundi mbalimbali wakiwemo maafisa hawa kwanza kuwahudumia kama wanachama, lakini pia kuwapa elimu ya matumizi ya huduma za PSSSF Kidijitali, ili iwe rahisi kwao kutekeleza majukumu yale yanayohusu taasisi zao na PSSSF” Alifafanua.

Naye Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa Magharibi, Bw. Thomas Labi, amewaeleza washiriki wa kikao kazi kilichofanyika mjini Bukoba kuwa, Mfuko umefanya uhuishaji wa mafao kwa Wastaafu wote kwa asilimia 2 na wastaafu wenye kima cha chini cha shilingi 150,000/- Pensheni yao imepanda hadi sh. 250,000/= kuanzia July 2025.

“Na si hivyo tu, Mstaafu akifariki, Mfuko unatoa sh. 500,000/= kama msaada wa mazishi. Lakini pia wategemezi wa mstaafu aliyefariki watalipwa mkupuo wa pensheni ya miezi 36.” Aliongeza.