
Daktari Bingwa wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu katika Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa (BMH), Dkt. Maxgama Ndosi, ameeleza kuwa hospitali hiyo imeanza kutoa matibabu mapya ya ubingwa wa juu yanayohusisha sindano maalumu katika uti wa mgongo, bila upasuaji.
"Leo tumeanzisha matibabu haya na tumeyafanya sisi wenyewe kama madaktari bingwa wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, tumefanikiwa kumhudumia mgonjwa wa kwanza na ametoka salama, matibabu haya yanahusisha sindano maalumu katika uti wa mgongo, na baada ya matibabu haya, maumivu ya mgongo huondoka kabisa"Amesema Dkt. Ndosi.
Ameongeza kuwa teknolojia hii mpya ina faida kubwa kwa wagonjwa, kwani haihusishi upasuaji na hivyo mgonjwa hahitaji kulazwa wodini.




"Matibabu haya yanamuondolea mgonjwa adha ya kukaa wodini, kwa kuwa yanatolewa kwa njia rahisi na salama. Baada ya kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza kuondoka siku hiyo hiyo"Amefafanua Dkt. Ndosi.
Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa Hospitali ya pili nchini kutoa matibabu haya na ya kwanza katika Kanda ya Kati, ikiendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuboresha huduma za ubingwa na ubingwa wa juu, tukio hili limekuja wakati hospitali hiyo ikiadhimisha miaka 10 tangu ianze kutoa huduma, ikiendelea kuwa kitovu cha ubunifu na maendeleo katika sekta ya Afya nchini.
