
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, imepanga kuiongezea fedha kampuni ya mbolea shilingi bilioni 40 kwa ajili ya kununua na kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakulima kote nchini.
Naibu Waziri wa Kilimo Mh Antony Mavunde, ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma ,wakati akijibu swali la Mbunge wa Kalambo Mh Josephat Kandege aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kuboresha utendaji kazi wa shirika la mbolea la taifa, ili kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakulima kwa ufanisi.
Mh Mavunde amesema kwa sasa serikali imeipatia kampuni ya mbolea ya taifa shilingi bilioni sita, ambazo umewezesha kampuni hiyo kununua jumla ya tani 4500 na kusambaza tani 3,851 za mbolea kwa wakulima 20,271.
Naibu Waziri huyo wa kilimo ameongeza kuwa mpango wa muda mrefu wa serikali ni kampuni hiyo kujenga kiwanda cha kuchanya mbolea, eneo la ekari 14.5 ambalo limepatikana kijiji cha Visegesi wilaya ya Kisarawe mkoa wa pwani ambapo ujenzi wake utaanza mwaka wa fedha 2023/2024.
