
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amekipandisha hadhi kwa Kituo cha Ununuzi wa Dhahabu cha Katoro kuwa soko kamili la dhahabu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa biashara ya madini na kuinua uchumi wa wachimbaji wadogo.
Mavunde amebainisha haya wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la mnada wa zamani Katoro, Geita, na kwamba hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio 16 makubwa yaliyopatikana katika sekta ya madini ndani ya miaka minne.
Amesema Mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa hadi kufikia asilimia 10.1, ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu, kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli kuelekea lengo la trilioni moja, pamoja na upatikanaji wa mitambo 15 ya kuchoronga kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Wachimbaji na wafanyabiashara wa madini waliokusanyika Katoro wamempongeza Rais Samia kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia sekta ya madini, hususan kwa kuweka mazingira rafiki ya uchimbaji na biashara.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Geita (GEREMA), Titus Kabuo, amesema lengo kuu la kusanyiko hilo ni kutoa pongezi kwa Rais kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha sekta ya madini na kuleta maendeleo kwa wachimbaji wadogo na uchumi wa nchi kwa ujumla.